Isaya Mlango 1 Isaiah

Isaya 1:1 Isaiah 1:1

Haya ni maono ya Isaya, mwana wa Amozi, aliyoyaona katika habari za Yuda na Yerusalemu, siku za Uzia na Yothamu na Ahazi na Hezekia, wafalme wa Yuda.

Isaya 1:2 Isaiah 1:2

Sikieni, enyi mbingu, tega sikio, Ee nchi, kwa maana Bwana amenena; Nimewalisha watoto na kuwalea, nao wameniasi.

Isaya 1:3 Isaiah 1:3

Ng'ombe amjua bwana wake, Na punda ajua kibanda cha bwana wake; Bali Israeli hajui, watu wangu hawafikiri.

Isaya 1:4 Isaiah 1:4

Ole wake, taifa lenye dhambi, watu wanaochukua mzigo wa uovu, wazao wa watenda mabaya, watoto wanaoharibu; wamemwacha Bwana, wamemdharau yeye aliye Mtakatifu wa Israeli, wamefarakana naye na kurudi nyuma.

Isaya 1:5 Isaiah 1:5

Mbona mnataka kupigwa hata sasa, hata mkazidi kuasi? Kichwa chote ni kigonjwa, moyo wote umezimia.

Isaya 1:6 Isaiah 1:6

Tangu wayo wa mguu hata kichwani hamna uzima ndani yake; bali jeraha na machubuko na vidonda vitokavyo usaha; havikufungwa, havikuzongwa-zongwa, wala havikulainishwa kwa mafuta.

Isaya 1:7 Isaiah 1:7

Nchi yenu ni ukiwa; miji yenu imeteketezwa kwa moto; nchi yenu, wageni wameila mbele ya macho yenu; nayo ni ukiwa, kana kwamba imeangamizwa na wageni.

Isaya 1:8 Isaiah 1:8

Na binti Sayuni ameachwa kama kibanda katika shamba la mizabibu, kama kipenu katika shamba la matango, kama mji uliohusuriwa.

Isaya 1:9 Isaiah 1:9

Kama Bwana wa majeshi asingalituachia mabaki machache sana, tungalikuwa kama Sodoma, tungalifanana na Gomora.

Isaya 1:10 Isaiah 1:10

Lisikieni neno la Bwana, enyi waamuzi wa Sodoma; tegeni masikio msikie sheria ya Mungu wetu, enyi watu wa Gomora.

Isaya 1:11 Isaiah 1:11

Huu wingi wa sadaka zenu mnazonitolea una faida gani? Asema Bwana. Nimejaa mafuta ya kafara za kondoo waume, na mafuta ya wanyama walionona; nami siifurahii damu ya ng'ombe wala ya wana-kondoo wala ya mbuzi waume.

Isaya 1:12 Isaiah 1:12

Mjapo ili kuonekana mbele zangu, ni nani aliyetaka neno hili mikononi mwenu, kuzikanyaga nyua zangu?

Isaya 1:13 Isaiah 1:13

Msilete tena matoleo ya ubatili; uvumba ni chukizo kwangu; mwezi mpya na sabato, kuita makutano; siyawezi maovu hayo na makutano ya ibada.

Isaya 1:14 Isaiah 1:14

Sikukuu zenu za mwezi mpya na karamu zenu zilizoamriwa, nafsi yangu yazichukia; mambo hayo yanilemea; nimechoka kuyachukua.

Isaya 1:15 Isaiah 1:15

Nanyi mkunjuapo mikono yenu, nitaficha macho yangu nisiwaone; naam, mwombapo maombi mengi, sitasikia; mikono yenu imejaa damu.

Isaya 1:16 Isaiah 1:16

Jiosheni, jitakaseni; ondoeni uovu wa matendo yenu usiwe mbele za macho yangu; acheni kutenda mabaya;

Isaya 1:17 Isaiah 1:17

jifunzeni kutenda mema; takeni hukumu na haki; wasaidieni walioonewa; mpatieni yatima haki yake; mteteeni mjane.

Isaya 1:18 Isaiah 1:18

Haya, njoni, tusemezane, asema Bwana. Dhambi zenu zijapokuwa nyekundu sana, zitakuwa nyeupe kama theluji; zijapokuwa nyekundu kama bendera, zitakuwa kama sufu.

Isaya 1:19 Isaiah 1:19

Kama mkikubali na kutii mtakula mema ya nchi;

Isaya 1:20 Isaiah 1:20

bali kama mkikataa na kuasi mtaangamizwa kwa upanga; maana kinywa cha Bwana kimenena haya.

Isaya 1:21 Isaiah 1:21

Mji huu uliokuwa mwaminifu umekuwaje kahaba! Yeye aliyejaa hukumu ya haki; haki ilikaa ndani yake, bali sasa wauaji!

Isaya 1:22 Isaiah 1:22

Fedha yako imekuwa takataka, divai yako imechanganywa na maji.

Isaya 1:23 Isaiah 1:23

Wakuu wako ni waasi, na rafiki za wevi; kila mtu hupenda rushwa, hufuata malipo; hawampatii yatima haki yake, wala maneno ya mjane hayawawasilii.

Isaya 1:24 Isaiah 1:24

Kwa hiyo, asema Bwana, Bwana wa majeshi, Mwenye enzi, wa Israeli, Nitapata faraja kwa hao wanipingao, nitatwaa kisasi kwa adui zangu;

Isaya 1:25 Isaiah 1:25

nami nitakuelekezea wewe mkono wangu, na kukutakasa takataka zako kabisa, na kukuondolea bati lako lote;

Isaya 1:26 Isaiah 1:26

nami nitarejeza upya waamuzi wako kama walivyokuwa hapo kwanza, na washauri wako kama hapo mwanzo; baada ya hayo utaitwa, Mji wa haki, mji mwaminifu.

Isaya 1:27 Isaiah 1:27

Sayuni itakombolewa kwa hukumu, na waongofu wake kwa haki.

Isaya 1:28 Isaiah 1:28

Lakini kuharibika kwao wakosao nao wenye dhambi kutatokea wakati mmoja, nao wamwachao Bwana watateketezwa.

Isaya 1:29 Isaiah 1:29

Kwa maana watatahayarika kwa sababu ya mialoni mliyoitamani, nanyi mtaaibishwa kwa sababu ya bustani mlizozichagua.

Isaya 1:30 Isaiah 1:30

Maana mtakuwa kama mwaloni ambao majani yake yakauka, na kama bustani isiyo na maji.

Isaya 1:31 Isaiah 1:31

Na mtu hodari atakuwa kama makumbi, na kazi yake kama cheche ya moto; nao watawaka pamoja, wala hapana atakayewazima.