Isaya Mlango 10 Isaiah

Isaya 10:1 Isaiah 10:1

Ole wao wawekao amri zisizo za haki, na waandishi waandikao maneno ya ushupavu;

Isaya 10:2 Isaiah 10:2

ili kumpotosha mhitaji asipate haki yake, na kuwanyang'anya maskini wa watu wangu haki yao; ili wajane wawe mateka yao, na kuwafanya yatima waliofiwa na baba zao kuwa mawindo yao!

Isaya 10:3 Isaiah 10:3

Nanyi mtafanya nini siku ya kujiliwa, na wakati wa uangamivu, utakaokuja kutoka mbali sana? Je! Mtamkimbilia nani mpate msaada? Na utukufu wenu mtauacha wapi?

Isaya 10:4 Isaiah 10:4

Watainama chini ya wafungwa tu, wataanguka chini yao waliouawa. Pamoja na hayo yote hasira yake haikugeukia mbali, lakini mkono wake umenyoshwa hata sasa.

Isaya 10:5 Isaiah 10:5

Ole wake Ashuru! Fimbo ya hasira yangu, ambaye gongo lililo mkononi mwake ni ghadhabu yangu!

Isaya 10:6 Isaiah 10:6

Nitamtuma juu ya taifa lenye kukufuru, nitampa maagizo juu ya watu wa ghadhabu yangu, ateke nyara, na kuchukua mateka, na kuwakanyaga kama matope ya njiani.

Isaya 10:7 Isaiah 10:7

Lakini hivyo sivyo akusudiavyo mwenyewe, wala sivyo moyo wake uwazavyo; maana katika moyo wake akusudia kuharibu, na kukatilia mbali mataifa, wala si mataifa machache.

Isaya 10:8 Isaiah 10:8

Maana asema, Je! Wakuu wangu si wote wafalme?

Isaya 10:9 Isaiah 10:9

Je! Kalno si kama Karkemishi? Hamathi si kama Arpadi? Samaria si kama Dameski?

Isaya 10:10 Isaiah 10:10

Kama vile mkono wangu ulivyofikilia falme za sanamu, ambazo sanamu zao za kuchongwa zilikuwa bora kuliko sanamu za Yerusalemu na za Samaria;

Isaya 10:11 Isaiah 10:11

je! Sitautenda Yerusalemu na sanamu zake vile vile kama nilivyoutenda Samaria na sanamu zake?

Isaya 10:12 Isaiah 10:12

Basi, itakuwa, Bwana atakapokuwa ameitimiza kazi yake yote juu ya mlima Sayuni na juu ya Yerusalemu, nitayaadhibu matunda ya kiburi cha moyo wake mfalme wa Ashuru, na majivuno ya macho yake.

Isaya 10:13 Isaiah 10:13

Kwa maana amesema, Kwa nguvu za mkono wangu nimetenda jambo hili, na kwa hekima yangu; maana mimi nina busara; nami nimeiondoa mipaka ya watu, nikaziteka akiba zao, nikawaangusha waketio juu ya viti vya enzi kama afanyavyo shujaa.

Isaya 10:14 Isaiah 10:14

Na mkono wangu umezitoa mali za mataifa kama katika kioto cha ndege; na kama vile watu wakusanyavyo mayai yaliyoachwa, ndivyo nilivyokusanya dunia yote; wala hapana aliyetikisa bawa, wala kufumbua kinywa, wala kulia.

Isaya 10:15 Isaiah 10:15

Je! Shoka lijisifu juu yake alitumiaye? Je! Msumeno ujitukuze juu yake auvutaye? Ingekuwa kana kwamba bakora ingewatikisa waiinuao, au fimbo ingemwinua yeye ambaye si mti.

Isaya 10:16 Isaiah 10:16

Kwa hiyo Bwana, Bwana wa majeshi, atawapelekea kukonda watu wake walionona; na badala ya utukufu wake kutawashwa kuteketea kama kuteketea kwa moto.

Isaya 10:17 Isaiah 10:17

Na mwanga wa Israeli utakuwa ni moto, na Mtakatifu wake atakuwa mwali wa moto; nao utateketeza na kula mbigili zake na miiba yake katika siku moja.

Isaya 10:18 Isaiah 10:18

Naye atauteketeza utukufu wa msitu wake, na wa shamba lake linalositawi, tangu nafsi hata nyama ya mwili, itakuwa kama vile afapo mtu aliye mgonjwa.

Isaya 10:19 Isaiah 10:19

Na miti ya msitu wake itakayosalia itakuwa michache, hata mtoto ataweza kuihesabu.

Isaya 10:20 Isaiah 10:20

Tena itakuwa katika siku hiyo mabaki ya Israeli, na hao waliopona wa nyumba ya Yakobo, hawatamtegemea tena yeye aliyewapiga, bali watamtegemea Bwana, Mtakatifu wa Israeli, kwa kweli.

Isaya 10:21 Isaiah 10:21

Mabaki, nao ni mabaki ya Yakobo, watamrudia Mungu, aliye mwenye nguvu.

Isaya 10:22 Isaiah 10:22

Maana watu wako, Ee Israeli, wajapokuwa wengi kama mchanga wa pwani, ni mabaki tu watakaorudi; kuangamiza kumekusudiwa, kunakofurika kwa haki.

Isaya 10:23 Isaiah 10:23

Kwa maana Bwana, Bwana wa majeshi, atayatimiza maangamizo yaliyokusudiwa katika nchi yote.

Isaya 10:24 Isaiah 10:24

Kwa hiyo Bwana, Bwana wa majeshi, asema hivi, Enyi watu wangu mkaao katika Sayuni, msiogope Ashuru, ingawa akupiga kwa fimbo, na kuliinua gongo lake juu yako, kwa namna ya Kimisri.

Isaya 10:25 Isaiah 10:25

Maana bado kitambo kidogo tu ghadhabu itakoma, na hasira yangu itageukia kuwaangamiza.

Isaya 10:26 Isaiah 10:26

Na Bwana wa majeshi ataamsha mjeledi juu yake, kama vile alivyopiga Midiani karibu na jabali la Orebu; na fimbo yake itakuwa juu ya bahari, naye ataiinua kwa namna ya Kimisri.

Isaya 10:27 Isaiah 10:27

Tena itakuwa katika siku hiyo mzigo wake utaondoka begani mwako, na nira yake shingoni mwako, nayo nira itaharibiwa, kwa sababu ya kutiwa mafuta.

Isaya 10:28 Isaiah 10:28

Amefika Ayathi; amepita kati ya Migroni; ameweka mizigo yake huko Mikmashi;

Isaya 10:29 Isaiah 10:29

wamevuka kivuko; wamekwenda kulala katika Geba; Rama unatetemeka; Gibea wa Sauli umekimbia.

Isaya 10:30 Isaiah 10:30

Piga kelele sana, Ee binti Galimu; sikiliza, Ee Laisha; ole wako, maskini Anathothi!

Isaya 10:31 Isaiah 10:31

Madmena ni mkimbizi; wenyeji wa Gebimu wamejikusanya wakimbie;

Isaya 10:32 Isaiah 10:32

siku hii ya leo atasimama huko Nobu; anatikisa mkono wake juu ya mlima wa binti Sayuni, mlima wa Yerusalemu.

Isaya 10:33 Isaiah 10:33

Angalia, Bwana, Bwana wa majeshi, atayakata matawi kwa nguvu za kutisha; nao walio warefu wa kimo watakatwa; na hao walioinuka wataangushwa chini;

Isaya 10:34 Isaiah 10:34

naye atavikata vichaka vya msitu kwa chuma; na Lebanoni utaanguka kwa mkono wake aliye mwenye uweza.