Isaya Mlango 61 Isaiah

Isaya 61:1 Isaiah 61:1

Roho ya Bwana MUNGU i juu yangu; kwa sababu Bwana amenitia mafuta niwahubiri wanyenyekevu habari njema; amenituma ili kuwaganga waliovunjika moyo, kuwatangazia mateka uhuru wao, na hao waliofungwa habari za kufunguliwa kwao.

Isaya 61:2 Isaiah 61:2

Kutangaza mwaka wa Bwana uliokubaliwa, na siku ya kisasi cha Mungu wetu; kuwafariji wote waliao;

Isaya 61:3 Isaiah 61:3

kuwaagizia hao waliao katika Sayuni, wapewe taji ya maua badala ya majivu, mafuta ya furaha badala ya maombolezo, vazi la sifa badala ya roho nzito; wapate kuitwa miti ya haki, iliyopandwa na Bwana, ili atukuzwe.

Isaya 61:4 Isaiah 61:4

Nao watajenga mahali pa kale palipoharibiwa, watapainua mahali palipokuwa ukiwa zamani, watatengeneza miji iliyoharibiwa, mahali palipoachwa kizazi baada ya kizazi.

Isaya 61:5 Isaiah 61:5

Na wageni watasimama na kulisha makundi yenu, na watu wa kabila nyingine watakuwa wakulima wenu, na watunzaji wa mizabibu yenu.

Isaya 61:6 Isaiah 61:6

Bali ninyi mtaitwa makuhani wa Bwana; watu watawaiteni wahudumu wa Mungu wetu; mtakula utajiri wa mataifa, na kujisifia utukufu wao.

Isaya 61:7 Isaiah 61:7

Badala ya aibu yenu mtapata maradufu, na badala ya fedheha wataifurahia sehemu yao; basi katika nchi yao watamiliki maradufu; furaha yao itakuwa ya milele.

Isaya 61:8 Isaiah 61:8

Maana mimi, Bwana, naipenda hukumu ya haki, nauchukia wivi na uovu; nami nitawalipa malipo katika kweli, nitaagana nao agano la milele.

Isaya 61:9 Isaiah 61:9

Na kizazi chao kitajulikana katika mataifa, na uzao wao katika kabila za watu; wote wawaonao watakiri ya kuwa wao ni kizazi kilichobarikiwa na Bwana.

Isaya 61:10 Isaiah 61:10

Nitafurahi sana katika Bwana, nafsi yangu itashangilia katika Mungu wangu; maana amenivika mavazi ya wokovu, amenifunika vazi la haki, kama bwana arusi ajipambavyo kwa kilemba cha maua, na kama bibi arusi ajipambavyo kwa vyombo vya dhahabu.

Isaya 61:11 Isaiah 61:11

Maana kama nchi itoavyo machipuko yake, na kama bustani ioteshavyo vitu vilivyopandwa ndani yake; ndivyo Bwana MUNGU atakavyootesha haki na sifa mbele ya mataifa yote.