Isaya Mlango 5 Isaiah

Isaya 5:1 Isaiah 5:1

Na nimwimbie mpenzi wangu wimbo wa mpenzi wangu katika habari za shamba lake la mizabibu. Mpenzi wangu alikuwa na shamba la mizabibu, Kilimani penye kuzaa sana;

Isaya 5:2 Isaiah 5:2

Akafanya handaki kulizunguka pande zote, Akatoa mawe yake, Akapanda ndani yake mzabibu ulio mzuri, Akajenga mnara katikati yake, Akachimba shinikizo ndani yake; Akatumaini ya kuwa utazaa zabibu, Nao ukazaa zabibu-mwitu.

Isaya 5:3 Isaiah 5:3

Na sasa, enyi wenyeji wa Yerusalemu, nanyi watu wa Yuda, amueni, nawasihi, kati ya mimi na shamba langu la mizabibu.

Isaya 5:4 Isaiah 5:4

Je! Ni kazi gani iliyoweza kutendeka ndani ya shamba langu la mizabibu nisiyoitenda? Basi, nilipotumaini ya kuwa litazaa zabibu, mbona lilizaa zabibu-mwitu?

Isaya 5:5 Isaiah 5:5

Haya basi, sasa nitawaambieni nitakalolitenda shamba langu la mizabibu; nitaondoa kitalu chake, nalo litaliwa; nitabomoa ukuta wake, nalo litakanyagwa;

Isaya 5:6 Isaiah 5:6

nami nitaliharibu; wala halitapogolewa wala kulimwa, bali litamea mbigili na miiba; nami nitayaamuru mawingu yasinyeshe mvua juu yake.

Isaya 5:7 Isaiah 5:7

Kwa maana shamba la mizabibu la Bwana wa majeshi ndilo nyumba ya Israeli, na watu wa Yuda ni mche wake wa kupendeza; akatumaini kuona hukumu ya haki, na kumbe! Aliona dhuluma; alitumaini kuona haki, na kumbe! Alisikia kilio.

Isaya 5:8 Isaiah 5:8

Ole wao waongezao nyumba baada ya nyumba, na kuweka shamba karibu na shamba, hata hapana nafasi tena, nanyi hamna budi kukaa peke yenu kati ya nchi!

Isaya 5:9 Isaiah 5:9

Bwana wa majeshi asema katika masikio yangu, Hakika majumba mengi yatakuwa ukiwa, naam, majumba makubwa, mazuri, yatakuwa hayana watu.

Isaya 5:10 Isaiah 5:10

Kwa maana shamba la mizabibu la eka kumi litatoa bathi moja tu, na homeri ya mbegu itatoa efa tu.

Isaya 5:11 Isaiah 5:11

Ole wao waamkao asubuhi na mapema, wapate kufuata kileo; wakishinda sana hata usiku wa manane mpaka mvinyo imewaka kama moto ndani yao!

Isaya 5:12 Isaiah 5:12

Na kinubi, na zeze, na matari, na filimbi, na mvinyo, zote ziko katika karamu zao; lakini hawaiangalii kazi ya Bwana wala kuyafikiri matendo ya mikono yake.

Isaya 5:13 Isaiah 5:13

Kwa sababu hiyo watu wangu wamechukuliwa mateka, kwa kukosa kuwa na maarifa; na watu wao wenye cheo wana njaa, na wengi wao waona kiu sana.

Isaya 5:14 Isaiah 5:14

Kwa hiyo kuzimu kumeongeza tamaa yake, kumefunua kinywa chake bila kiasi; na utukufu wao, na wingi wao, na ghasia yao, naye pia afurahiye miongoni mwao, hushuka na kuingia humo.

Isaya 5:15 Isaiah 5:15

Na mtu mnyonge ainamishwa, na mtu mkubwa amedhilika, na macho yao walioinuka hunyenyekezwa,

Isaya 5:16 Isaiah 5:16

bali Bwana wa majeshi ametukuzwa katika hukumu, na Mungu aliye Mtakatifu ametakaswa katika haki.

Isaya 5:17 Isaiah 5:17

Ndipo wana-kondoo watakapolisha kama katika malisho yao wenyewe, na mahali pao waliowanda, palipoachwa ukiwa, wageni watakula.

Isaya 5:18 Isaiah 5:18

Ole wao wavutao uovu kwa kamba za ubatili, na dhambi kama kwa kamba za gari!

Isaya 5:19 Isaiah 5:19

Wasema, Na afanye haraka, aihimize kazi yake, tupate kuiona; na likaribie shauri lake aliye Mtakatifu wa Israeli, tupate kuliona.

Isaya 5:20 Isaiah 5:20

Ole wao wasemao kwamba uovu ni wema, na kwamba wema ni uovu; watiao giza badala ya nuru, na nuru badala ya giza; watiao uchungu badala ya utamu, na utamu badala ya uchungu!

Isaya 5:21 Isaiah 5:21

Ole wao walio wenye hekima katika macho yao wenyewe, na wenye busara katika fikira zao wenyewe!

Isaya 5:22 Isaiah 5:22

Ole wao walio hodari kunywa kileo chenye nguvu, watu waume wenye nguvu kuchanganya vileo;

Isaya 5:23 Isaiah 5:23

wampao haki mwenye uovu, ili wapewe ijara, na kumwondolea mwenye haki haki yake!

Isaya 5:24 Isaiah 5:24

Kwa hiyo kama vile mwali wa moto uteketezavyo mabua makavu, na kama manyasi makavu yaangukavyo katika mwali wa moto; kadhalika shina lao litakuwa kama ubovu, na ua lao litapeperushwa juu kama mavumbi; kwa sababu wameikataa sheria ya Bwana wa majeshi, na kulidharau neno lake aliye Mtakatifu wa Israeli.

Isaya 5:25 Isaiah 5:25

Kwa sababu hiyo hasira ya Bwana imewaka juu ya watu wake, naye amenyosha mkono wake juu yao; akawapiga, navyo vilima vilitetemeka, na mizoga yao ilikuwa kama takataka katika njia kuu. Pamoja na hayo yote hasira yake haikugeukia mbali, lakini mkono wake umenyoshwa hata sasa.

Isaya 5:26 Isaiah 5:26

Naye atawatwekea bendera mataifa toka mbali, Naye atawapigia miunzi tokea mwisho wa nchi; Na tazama, watakuja mbio mbio upesi sana.

Isaya 5:27 Isaiah 5:27

Miongoni mwao hakuna achokaye wala kukwaa; Hakuna asinziaye wala kulala usingizi; Wala mshipi wa viuno vyao hautalegea. Wala ukanda wa viatu vyao hautakatika;

Isaya 5:28 Isaiah 5:28

Mishale yao ni mikali, na pindi zao zote zimepindika; Kwato za farasi zao zitahesabika kama gumegume; Na gurudumu zao kama kisulisuli;

Isaya 5:29 Isaiah 5:29

Ngurumo yao itakuwa kama ya simba; Watanguruma kama wana-simba; Naam, watanguruma na kukamata mateka, Na kuyachukua na kwenda zao salama, Wala hakuna mtu atakayeokoa.

Isaya 5:30 Isaiah 5:30

Nao watanguruma juu yao siku hiyo Kama ngurumo ya bahari; Na mtu akiitazama nchi, ataona giza na dhiki Nayo nuru imetiwa giza katika mawingu yake.