Isaya Mlango 56 Isaiah

Isaya 56:1 Isaiah 56:1

Bwana asema hivi, Shikeni hukumu, mkatende haki; kwa maana wokovu wangu u karibu kuja, na haki yangu kufunuliwa.

Isaya 56:2 Isaiah 56:2

Heri afanyaye haya, na mwanadamu ayashikaye sana; azishikaye sabato asizivunje, auzuiaye mkono wake usifanye uovu wo wote.

Isaya 56:3 Isaiah 56:3

Wala mgeni, aambatanaye na Bwana, asiseme hivi, Hakika yake Bwana atanitenga na watu wake; wala towashi asiseme, Mimi ni mti mkavu.

Isaya 56:4 Isaiah 56:4

Kwa maana Bwana awaambia hivi matowashi, wanaozishika sabato zangu, na kuyachagua mambo yanipendezayo, na kulishika sana agano langu;

Isaya 56:5 Isaiah 56:5

Nitawapa hawa nyumbani mwangu, na ndani ya kuta zangu, kumbukumbu na jina, lililo jema kuliko kuwa na wana na binti; nitawapa jina lidumulo milele, lisilokatiliwa mbali.

Isaya 56:6 Isaiah 56:6

Na wageni, walioandamana na Bwana ili wamhudumu, na kulipenda jina la Bwana, kuwa watumishi wake; kila aishikaye sabato asiivunje, na kulishika sana agano langu;

Isaya 56:7 Isaiah 56:7

Nitawaleta hao nao hata mlima wangu mtakatifu, na kuwafurahisha katika nyumba yangu ya sala; makafara yao na dhabihu zao zitakubaliwa juu ya madhabahu zangu; kwa maana nyumba yangu itaitwa nyumba ya sala kwa mataifa yote.

Isaya 56:8 Isaiah 56:8

Bwana MUNGU, akusanyaye waliofukuzwa katika Israeli asema, Pamoja na hayo nitamkusanyia na wengine, zaidi ya hao walio wake waliokusanywa.

Isaya 56:9 Isaiah 56:9

Enyi hayawani wote wa nyikani, njoni, Mle, enyi hayawani wote wa mwituni.

Isaya 56:10 Isaiah 56:10

Walinzi wake ni vipofu, wote pia hawana maarifa; wote ni mbwa walio bubu, hawawezi kulia; huota ndoto, hulala, hupenda usingizi.

Isaya 56:11 Isaiah 56:11

Naam, mbwa hao wana choyo sana, hawashibi kamwe; na hao ni wachungaji wasioweza kufahamu neno; wote pia wamegeuka upande, wazifuate njia zao wenyewe, kila mmoja kwa faida yake, toka pande zote.

Isaya 56:12 Isaiah 56:12

Husema, Njoni, nitaleta divai, Na tunywe sana kileo; Na kesho itakuwa kama leo, Sikukuu kupita kiasi.