Isaya Mlango 58 Isaiah

Isaya 58:1 Isaiah 58:1

Piga kelele, usiache, Paza sauti yako kama tarumbeta; Uwahubiri watu wangu kosa lao, Na nyumba ya Yakobo dhambi zao.

Isaya 58:2 Isaiah 58:2

Walakini wanitafuta kila siku; hupenda kujua njia zangu; kama vile taifa waliotenda haki, wasioacha sheria ya Mungu wao, hutaka kwangu amri za haki; hufurahi kumkaribia Mungu.

Isaya 58:3 Isaiah 58:3

Husema, Mbona tumefunga, lakini huoni? Mbona tumejitaabisha nafsi zetu, lakini huangalii? Fahamuni, siku ya kufunga kwenu mnatafuta anasa zenu wenyewe, na kuwalemea wote watendao kazi kwenu.

Isaya 58:4 Isaiah 58:4

Tazama, ninyi mwafunga mpate kushindana na kugombana, na kupiga kwa ngumi ya uovu. Hamfungi siku hii ya leo hata kuisikizisha sauti yenu juu.

Isaya 58:5 Isaiah 58:5

Je! Kufunga namna hii ni saumu niliyoichagua mimi? Je! Ni siku ya mtu kujitaabisha nafsi yake? Ni kuinama kichwa kama unyasi, na kutanda nguo za magunia na majivu chini yake? Je! Utasema ni siku ya kufunga, na ya kukubaliwa na Bwana?

Isaya 58:6 Isaiah 58:6

Je! Saumu niliyoichagua, siyo ya namna hii? Kufungua vifungo vya uovu, kuzilegeza kamba za nira, kuwaacha huru walioonewa, na kwamba mvunje kila nira?

Isaya 58:7 Isaiah 58:7

Je! Siyo kuwagawia wenye njaa chakula chako, na kuwaleta maskini waliotupwa nje nyumbani kwako? Umwonapo mtu aliye uchi, umvike nguo; wala usijifiche na mtu mwenye damu moja nawe?

Isaya 58:8 Isaiah 58:8

Ndipo nuru yako itakapopambazuka kama asubuhi, na afya yako itatokea mara; na haki yako itakutangulia; utukufu wa Bwana utakufuata nyuma ukulinde.

Isaya 58:9 Isaiah 58:9

Ndipo utaita, na Bwana ataitika; utalia, naye atasema, Mimi hapa. Kama ukiiondoa nira; isiwepo kati yako, wala kunyosha kidole, wala kunena maovu;

Isaya 58:10 Isaiah 58:10

na kama ukimkunjulia mtu mwenye njaa nafsi yako, na kuishibisha nafsi iliyoteswa; ndipo nuru yako itakapopambazuka gizani; na kiwi chako kitakuwa kama adhuhuri.

Isaya 58:11 Isaiah 58:11

Naye Bwana atakuongoza daima, ataishibisha nafsi yako mahali pasipokuwa na maji, na kuitia nguvu mifupa yako; nawe utakuwa kama bustani iliyotiwa maji, na kama chemchemi ambayo maji yake hayapungui.

Isaya 58:12 Isaiah 58:12

Na watu wako watapajenga mahali palipokuwa ukiwa; utaiinua misingi ya vizazi vingi; nawe utaitwa, Mwenye kutengeneza mahali palipobomoka; na, Mwenye kurejeza njia za kukalia.

Isaya 58:13 Isaiah 58:13

Kama ukigeuza mguu wako usihalifu sabato, usifanye anasa yako siku ya utakatifu wangu; ukiita sabato siku ya furaha, na siku takatifu ya Bwana yenye heshima; ukiitukuza, kwa kutokuzifanya njia zako mwenyewe, wala kuyatafuta yakupendezayo, wala kusema maneno yako mwenyewe;

Isaya 58:14 Isaiah 58:14

ndipo utakapojifurahisha katika Bwana; nami nitakupandisha mahali pa nchi palipoinuka; nitakulisha urithi wa Yakobo baba yako; kwa maana kinywa cha Bwana kimenena hayo.