Isaya Mlango 6 Isaiah

Isaya 6:1 Isaiah 6:1

Katika mwaka ule aliokufa mfalme Uzia nalimwona Bwana ameketi katika kiti cha enzi, kilicho juu sana na kuinuliwa sana, na pindo za vazi lake zikalijaza hekalu.

Isaya 6:2 Isaiah 6:2

Juu yake walisimama maserafi; kila mmoja alikuwa na mabawa sita; kwa mawili alifunika uso wake, na kwa mawili alifunika miguu yake, na kwa mawili aliruka.

Isaya 6:3 Isaiah 6:3

Wakaitana, kila mmoja na mwenzake, wakisema, Mtakatifu, Mtakatifu, Mtakatifu, ni Bwana wa majeshi; dunia yote imejaa utukufu wake.

Isaya 6:4 Isaiah 6:4

Na misingi ya vizingiti ikatikisika kwa sababu ya sauti yake aliyelia, nayo nyumba ikajaa moshi.

Isaya 6:5 Isaiah 6:5

Ndipo niliposema, Ole wangu! Kwa maana nimepotea; kwa sababu mimi ni mtu mwenye midomo michafu, nami ninakaa kati ya watu wenye midomo michafu; na macho yangu yamemwona Mfalme, Bwana wa majeshi.

Isaya 6:6 Isaiah 6:6

Kisha mmoja wa maserafi wale akaruka akanikaribia; naye alikuwa na kaa la moto mkononi mwake, ambalo alikuwa amelitwaa kwa makoleo toka juu ya madhabahu;

Isaya 6:7 Isaiah 6:7

akanigusa kinywa changu kwa kaa hilo, akaniambia, Tazama, hili limekugusa midomo yako, na uovu wako umeondolewa, na dhambi yako imefunikwa.

Isaya 6:8 Isaiah 6:8

Kisha nikaisikia sauti ya Bwana, akisema, Nimtume nani, naye ni nani atakayekwenda kwa ajili yetu? Ndipo niliposema, Mimi hapa, nitume mimi.

Isaya 6:9 Isaiah 6:9

Naye akaniambia, Enenda, ukawaambie watu hawa, Fulizeni kusikia, lakini msifahamu; fulizeni kutazama, lakini msione.

Isaya 6:10 Isaiah 6:10

Uunoneshe moyo wa watu hawa, ukayatie uzito masikio yao, ukayafumbe macho yao; wasije wakaona kwa macho yao, na kusikia kwa masikio yao, na kufahamu kwa mioyo yao, na kurejea na kuponywa.

Isaya 6:11 Isaiah 6:11

Ndipo nilipouliza, Ee Bwana, hata lini? Naye akanijibu, Hata miji itakapokuwa ukiwa, haina wenyeji, na nyumba zitakapokuwa hazina watu, na nchi hii itakapokuwa ganjo kabisa;

Isaya 6:12 Isaiah 6:12

hata Bwana atakapowahamisha watu waende mbali sana, na mahame yatakapokuwa mengi ndani ya nchi.

Isaya 6:13 Isaiah 6:13

Na ijapokuwa imebaki sehemu moja katika sehemu kumi ndani yake, italiwa hii nayo; kama mvinje na kama mwaloni, ambao shina lake limebaki, ingawa imekatwa; kadhalika mbegu takatifu ndiyo shina lake.