Ayabu Mlango 20 Job

Ayabu 20:1 Job 20:1

Ndipo Sofari, Mnaamathi, akajibu, na kusema,

Ayabu 20:2 Job 20:2

Kwa hiyo mawazo yangu hunipa jawabu, Kwa ajili ya haraka niliyo nayo ndani yangu.

Ayabu 20:3 Job 20:3

Nimesikia maonyo yanayonitahayarisha, Nayo roho ya ufahamu wangu hunijibu.

Ayabu 20:4 Job 20:4

Je! Hujui neno hili tangu zamani za kale, Tangu wanadamu kuwekwa juu ya nchi,

Ayabu 20:5 Job 20:5

Ya kuwa shangwe ya waovu ni kwa muda kidogo, Na furaha ya wapotovu ni ya dakika moja tu?

Ayabu 20:6 Job 20:6

Ujapopanda ukuu wake mpaka mbinguni, Na kichwa chake kufikilia mawinguni;

Ayabu 20:7 Job 20:7

Hata hivyo ataangamia milele kama mavi yake mwenyewe; Hao waliomwona watasema, Yuko wapi?

Ayabu 20:8 Job 20:8

Ataruka mfano wa ndoto, asionekane; Naam, atafukuzwa kama maono ya usiku,

Ayabu 20:9 Job 20:9

Jicho lililomwona halitamwona tena; Wala mahali pake hapatamtazama tena.

Ayabu 20:10 Job 20:10

Watoto wake watataka fadhili kwa maskini, Na mikono yake itarudisha mali yake.

Ayabu 20:11 Job 20:11

Mifupa yake imejaa ujana wake, Lakini utalala nchi naye mavumbini.

Ayabu 20:12 Job 20:12

Ingawa uovu una tamu kinywani mwake, Ingawa auficha chini ya ulimi wake;

Ayabu 20:13 Job 20:13

Ingawa auhurumia, asikubali kuuacha uende zake. Lakini akaushika vivyo kinywani mwake;

Ayabu 20:14 Job 20:14

Hata hivyo chakula chake matumboni mwake kinabadilika, Kimekuwa ni nyongo za majoka ndani yake.

Ayabu 20:15 Job 20:15

Amemeza mali, naye atayatapika tena; Mungu atayatoa tumboni mwake.

Ayabu 20:16 Job 20:16

Ataamwa sumu ya majoka; Na ulimi wa fira utamwua.

Ayabu 20:17 Job 20:17

Hataiangalia hiyo mito ya maji, Vile vijito vilivyojaa asali na siagi.

Ayabu 20:18 Job 20:18

Aliyoyataabikia kazi atayarudisha, asiyameze; Kwa mali aliyoyapata, hatafurahi.

Ayabu 20:19 Job 20:19

Kwa maana amewaonea na kuwaacha maskini; Amenyang'anya nyumba kwa jeuri, wala hataijenga.

Ayabu 20:20 Job 20:20

Kwa sababu hakujua utulivu ndani yake, Hataponya cho chote katika hicho alichokifurahia.

Ayabu 20:21 Job 20:21

Hakikusalia kitu asichokula; Kwa hiyo kufanikiwa kwake hakutadumu.

Ayabu 20:22 Job 20:22

Katika kujaa kwa wingi wake atakuwa katika dhiki; Mkono wa kila anayesumbuliwa utamjia.

Ayabu 20:23 Job 20:23

Hapo atakapo kulijaza tumbo lake, Mungu atamtupia ukali wa ghadhabu zake, Na kuunyesha juu yake akiwa anakula.

Ayabu 20:24 Job 20:24

Ataikimbia silaha ya chuma, Na uta wa shaba utamchoma kwa pili.

Ayabu 20:25 Job 20:25

Yeye autoa, nao watoka mwilini mwake; Naam, ncha ing'aayo yatoka katika nyongo yake; Vitisho viko juu yake.

Ayabu 20:26 Job 20:26

Giza lote linawekwa kwa ajili ya hazina zake; Moto ambao haukuvuviwa na mtu utamla; Utayateketeza yaliyosalia hemani mwake.

Ayabu 20:27 Job 20:27

Mbingu zitafunua wazi uovu wake, Nayo nchi itainuka kinyume chake.

Ayabu 20:28 Job 20:28

Maongeo ya nyumba yake yataondoka, Yatamwagika mbali katika siku ya ghadhabu zake.

Ayabu 20:29 Job 20:29

Hii ndiyo sehemu ya mtu mwovu itokayo kwa Mungu, Na urithi aliowekewa na Mungu.