Ayabu Mlango 30 Job

Ayabu 30:1 Job 30:1

Lakini sasa hao walio wadogo wangu hunifanyia mzaha, Ambao baba zao niliwadharau hata kuwaweka na mbwa wa kundi langu.

Ayabu 30:2 Job 30:2

Naam, uwezo wa mikono yao utanifaa nini? Watu ambao nguvu zao zimekoma.

Ayabu 30:3 Job 30:3

Wamekonda kwa uhitaji na njaa; Huguguna nchi kavu, penye giza la ukiwa na uharibifu.

Ayabu 30:4 Job 30:4

Hung'oa mboga ya chumvi kwenye kichaka; Na mizizi ya mretemu ni chakula chao.

Ayabu 30:5 Job 30:5

Hufukuzwa watoke kati ya watu; Huwapigia kelele kama kumpigia mwivi.

Ayabu 30:6 Job 30:6

Lazima hukaa katika mianya ya mabonde, Katika mashimo ya nchi na ya majabali.

Ayabu 30:7 Job 30:7

Hulia kama punda vichakani; Hukusanyika chini ya upupu.

Ayabu 30:8 Job 30:8

Wao ni wana wa wapumbavu, naam, watoto wa wahuni; Walifukuzwa kwa mijeledi watoke katika nchi.

Ayabu 30:9 Job 30:9

Na sasa mimi nimekuwa wimbo wao, Naam, nimekuwa simo kwao.

Ayabu 30:10 Job 30:10

Wao hunichukia, na kujitenga nami, Hawaachi kunitemea mate usoni.

Ayabu 30:11 Job 30:11

Kwani ameilegeza kamba yake, na kunitesa, Wala hawajizuii tena mbele yangu.

Ayabu 30:12 Job 30:12

Kwa mkono wangu wa kuume huinuka kundi; Huisukuma miguu yangu kando, Na kunipandishia njia zao za uharibifu.

Ayabu 30:13 Job 30:13

Waiharibu njia yangu, Wauzidisha msiba wangu, Watu wasio na msaidizi.

Ayabu 30:14 Job 30:14

Wanijilia kama wapitao katika ufa mpana; Katikati ya magofu wanishambulia.

Ayabu 30:15 Job 30:15

Vitisho vimenigeukia; Huifukuza heshima yangu kama upepo; Na kufanikiwa kwangu kumepita kama wingu.

Ayabu 30:16 Job 30:16

Sasa nafsi yangu inamwagika ndani yangu; Siku za mateso zimenishika.

Ayabu 30:17 Job 30:17

Wakati wa usiku mifupa yangu huchomeka ndani yangu, Na maumivu yanayonitafuna hayapumziki.

Ayabu 30:18 Job 30:18

Kwa ugonjwa wangu kuwa na nguvu nyingi Mavazi yangu yameharibika; Hunikaza kama shingo ya kanzu yangu.

Ayabu 30:19 Job 30:19

Yeye amenibwaga topeni, Nami nimekuwa kama mavumbi na majivu.

Ayabu 30:20 Job 30:20

Nakulilia wewe, wala huniitikii; Nasimama, nawe wanitazama tu.

Ayabu 30:21 Job 30:21

Wewe umegeuka kuwa mkali kwangu; Nawe waniudhi kwa uweza wa mkono wako.

Ayabu 30:22 Job 30:22

Waniinua juu hata upeponi, na kunipandisha juu yake; Nawe waniyeyusha katika dhoruba.

Ayabu 30:23 Job 30:23

Kwani najua kuwa utanileta hata kifoni, Niifikilie nyumba waliyoandikiwa wenye uhai wote.

Ayabu 30:24 Job 30:24

Je! Mtu katika kuanguka kwake hanyoshi mkono? Na kulilia msaada katika msiba wake?

Ayabu 30:25 Job 30:25

Je! Mimi sikulia kwa ajili ya huyo aliyekuwa katika taabu? Nafsi yangu, je! Haikusononeka kwa ajili ya wahitaji?

Ayabu 30:26 Job 30:26

Hapo nilipotazamia mema, ndipo yakaja mabaya; Nami nilipongojea mwanga, likaja giza.

Ayabu 30:27 Job 30:27

Matumbo yangu yatokota, wala hayaachi; Siku za taabu zimenijilia.

Ayabu 30:28 Job 30:28

Naenda nikiomboleza pasipo jua; Nasimama katika mkutano, na kuulilia msaada.

Ayabu 30:29 Job 30:29

Mimi ni ndugu yao mbwa-mwitu, Ni mwenzao mbuni.

Ayabu 30:30 Job 30:30

Ngozi yangu ni nyeusi, nayo yanitoka, Na mifupa yangu imeteketea kwa hari.

Ayabu 30:31 Job 30:31

Kwa hiyo kinanda changu kimegeuzwa kuwa maombolezo, Na filimbi yangu kuwa sauti yao waliao.